1 Kings 19

Ilya Akimbilia Horebu

1 aAhabu akamwambia Yezebeli kila kitu Ilya alichokuwa amefanya na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga. 2 bHivyo Yezebeli akamtuma mjumbe kwa Ilya, kusema, “Hao miungu initendee hivyo na kuzidi, kama kufikia kesho wakati kama huu sitaifanya roho yako kama mmojawapo wa hao manabii.”

3 cIlya aliogopa, na akakimbia kuokoa maisha yake. Alipofika Beer-Sheba katika Yuda, akamwacha mtumishi wake huko, 4 dlakini yeye mwenyewe akatembea mwendo wa kutwa nzima katika jangwa. Akafika kwenye mti wa mretemu, akakaa chini yake na kuomba ili afe. Akasema, “Yatosha sasa, Bwana, ondoa roho yangu, kwani mimi si bora kuliko baba zangu.” 5 eKisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi.

Mara malaika akamgusa na akamwambia, “Inuka na ule.”
6Akatazama pande zote, napo hapo karibu na kichwa chake palikuwepo mkate uliookwa kwenye makaa ya moto na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena.

7Yule malaika wa Bwana akaja tena mara ya pili, akamgusa akamwambia, “Inuka na ule, kwa kuwa safari ni ndefu kwako.” 8 fKwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana mpaka akafika Horebu, mlima wa Mungu. 9Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule.

Bwana Amtokea Ilya

Nalo neno la Bwana likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Ilya?”

10 gAkajibu, “Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote. Waisraeli wamelikataa Agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi, mimi peke yangu, niliyebaki, nao sasa wananitafuta ili waniangamize.” 11 h Bwana akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za Bwana, kwa kuwa Bwana yu karibu kupita hapo.”

Kisha upepo mwingi na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za Bwana, lakini Bwana hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la nchi, lakini Bwana hakuwamo kwenye lile tetemeko.
12Baada ya tetemeko la nchi ukaja moto, lakini Bwana hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunong’ona. 13 iIlya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mdomo wa pango.

Kisha ile sauti ikamwambia, “Ilya, unafanya nini hapa?”

14Akajibu, “Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote. Waisraeli wamelikataa Agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi, mimi peke yangu, niliyebaki, nao sasa wananitafuta ili waniangamize.”

15 j Bwana akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Wakati utakapofika huko, mtie Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu
Yaani Shamu (ambayo leo ni Syria).
16Pia mtie mafuta Yehu mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umtie Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola mafuta awe nabii badala yako. 17 lYehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. 18 mHata sasa nimeweka akiba watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.”

Wito Wa Al-Yasa

19Hivyo Ilya akaondoka kutoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akapita karibu naye, akamrushia vazi lake. 20 nKisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.”

Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekutendea nini?”

21Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.
Copyright information for SwhKC